HABARI: Wakili ameieleza Mahakama sababu ya mashtaka dhidi ya Mbowe, Viongozi CHADEMA yafutwe
Leo May 16, 2018 Upande wa utetezi katika kesi ya uchochezi inayowakabili Viongozi wa CHADEMA akiwemo Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe umeiomba mahakama kuwafutia mashtaka washtakiwa kwa kuwa yana mapungufu kisheria.
Maombi hayo yamewasilishwa na Wakili wa utetezi, Peter Kibatala mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Wilbard Mashauri wakati kesi hiyo ilipoitishwa ili washtakiwa wasomewe maelezo ya awali (Ph).
Katika maombi hayo ambayo Kibatala aliwasilisha mapingamizi 8, ambapo amedai, kibali cha DPP kina upungufu wa kisheria kwa sababu haioneshi imetolewa kwa mashtaka yapi.
Pia hati ya mashtaka imewataja majina washtakiwa wote bila ya kufafanua, pia imetaja kifungu cha sheria ambacho washtakiwa wameshtakiwa nacho.
Katika pingamizi hilo, Kibatala amedai kuwa kibali kilichowasilishwa mahakamani hapo kwa maana hiyo mashtaka dhidi ya washtakiwa yamepelekwa mahakamani hapo bila ridhaa ya DPP.
Aidha Kibatala amedai kuwa, iwapo kama mahakama itashindwa kuifuta hati nzima ya mashtaka yanayowakabili washtakiwa hao basi iyafutilie mbali mashtaka ambayo yana mapungufu kisheria, ikiwamo shtaka la nne, latano, la sita na la saba.
Akijibu hoja hizo, Wakili wa serikali Mkuu, Paul Kadushi aliiomba mahakama kuyatupilia mbali mapingamizi yote hayo ya upande wa utetezi kwa kuwa hayana mashiko kisheria.
Kuhusu kibali cha DPP kinachoipa mahakama ridhaa ya kusikiliza kesi hiyo, Kadushi amedai kuwa hakuna uamuzi wowote ulioweka msingi kwamba ni lazima kiwepo na nini hakipaswi kuwepo.

0 komentar:
Post a Comment